Wednesday, July 27, 2016

SISI HATUMO MIONGONI MWAO WANAOPOTEA MAANA TUNAYE YESU KRISTO.

Mtumishi Peter Michael Mabula

SISI HATUMO MIONGONI MWAO WANAOPOTEA MAANA TUNAYE YESU KRISTO.
 
BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze ujumbe special kabisa wa neno la MUNGU.

Waebrania 10:39 '' Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu. ''

Wanaopotea ni wale wanaomkataa BWANA YESU kama Mwokozi wao.
Wanaopotea ni wale wanaokataa Wokovu wa KRISTO.
Wanaopotea ni wale ambao hawaishi maisha matakatifu ya wokovu.
Wanaopotea ni watenda dhambi wasiotaka kutubu.
Wanaopotea ni wazinzi na waasherati ambao hawana mpango wa kutubia uovu wao huo na kuuacha.
Sisi tuliookoka hatumo miongoni mwao wanaopotea maana tunamtii KRISTO na Neno lake.
 
Luka 19:10 ''Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. ''

BWANA YESU alikuja kuokoa kile kilichopotea ambacho ni mwanadamu, lakini mwanadamu huyo akimkataa BWANA YESU ataendelea kupotea na mwisho wa waliopotea ni ziwa la moto.

Injili ya KRISTO inawahitaji wanadamu wote.
Injili ya KRISTO inaweza kuwaokoa wanadamu wote ila tu wanadamu hao wanatakiwa kuufuata uzima kwa kumpokea BWANA YESU kama BWANA na Mwokozi wao.

2 Kor 4:3-6 '' Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii(shetani) amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU. Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali KRISTO YESU ya kuwa ni BWANA; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya YESU. Kwa kuwa MUNGU, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng'aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa MUNGU katika uso wa YESU KRISTO.''

Kama injili ni ngeni basi ni ngeni tu kwa hao wanaopotea.
Kama toba ni jambo gumu basi ni gumu tu kwa hao wanaopotea.
Kama kuacha dhambi ni haiwezekani basi haiwezekani tu kwa hao wanaopotea wasio na haja ya kutubu.
Ndugu, usikubali kupotea bali okoka na anza upya na BWANA YESU mwenye uzima wako wa milele.
Kama ulikuwa umepotea basi nakuomba geuka leo kwa kumpokea BWANA YESU nayeokoa.
Sisi tuliookoka hatumo miongoni mwao wanaopotea maana tunamtii KRISTO na Neno lake.

1 Kor 1:18 '' Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya MUNGU.''

Waliopotea ni wale wanaokataa kazi ya Mwokozi YESU pale msalabani.
Wanaopotea ni wachawi na waganga wanaotumainia kazi zao feki wakiwa hawana haja ya kutubu na kuacha dhambi.
Wanaopotea ni wale wanaopingana na Neno la MUNGU yaani Biblia.
Sisi sio miongoni mwao wanaopotea maana tunaye KRISTO YESU Mwokozi wetu..
Waliopotea ni wale walio na juhudi katika maovu na mambo ya kidunia, wakiwa hawataki wokovu wa BWANA YESU.
Sisi sio miongoni mwao wanaopotea maana sisi tunaishi maisha matakatifu katika BWANA YESU.
Wanapotea ni wale wasio mtii MUNGU.
Wanapotea ni wale Wasio na wokovu wa KRISTO.
Wanapotea ni wale Wachawi na waongo.
Wanapotea ni wale wanaoenda kwa waganga wa kienyeji.
Wanapotea ni wale wanaoabudu sanamu.
Wanapotea ni wale wanaosujudia mawe na miti.
Wanapotea ni wale waasherati wasio na haja ya kutubu.
Wanapotea ni wale wezi na majambazi.
Wanapotea ni wale watoa rushwa na wapokea rushwa wasio tubu.
Wanapotea ni wale mafisadi na walaghai.
Wanapotea ni wale Wasaliti wa ndoa zao.
Wanapotea ni wale Wasengenyaji na wachonganishi.
Wanapotea ni wale waongo na mashoga.
Wanapotea ni wale walawiti na wafiraji na wafirwaji.
Wanaopotea ni wale wanaooa mke zaidi ya mmoja.
wanaopotea ni watenda dhambi wasio na haja ya kuja kwa YESU kuokoka na kutubu ili wasamehewe.
Sisi sio miongoni mwao wanaopotea maana sisi tunaishi maisha matakatifu katika BWANA YESU.
Sisi sio miongoni mwao wanaopotea maana KRISTO ndiye mwokozi wa maisha yetu.

BWANA YESU alikuja kuokoa kile kilichopotea ambacho ni mwanadamu, lakini mwanadamu huyo akimkataa BWANA YESU ataendelea kupotea na mwisho wa waliopotea ni ziwa la moto.
Ndugu, usikubali kuwa miongoni mwao wanaopotea.
BWANA YESU anatamani aseme siku ile ya mwisho kwamba ''Karibu mtumwa mwema na Mwaminifu''
Ndugu, usikubali kushawishiwa na mwanadamu wa aina yeyote kwamba eti umwache YESU.
Kumuacha BWANA YESU ni kuuacha uzima.
Sisi tuliookoka hatumo miongoni mwao wanaopotea maana tunamtii KRISTO na Neno lake.
Zaburi 1:6 ''Kwa kuwa BWANA anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Tuesday, July 5, 2016

FUTA UONGO UNAOKAA KATIKA MAISHA YAKO.

Mwinjilisti Peter M Mabula.


BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Neno ''Uongo'' maana yake ni tabia ya kudanganya pia unaweza kusema kwamba ''uongo'' ni kusema jambo ambalo sio la Kweli.
Uongo una mtoto anayeitwa uzushi.
''Uzushi'' maana yake hali ya kuzua mambo ambayo sio ya kweli.
Uongo ni bidhaa ya shetani inayowatesa watu wengi sana.
Kuna watu wanateseka kwa kusemewa uongo, na kuna wanaoteseka kwa sababu wanatamani kuiacha dhambi ya uongo lakini bado hawajafanikiwa kuuacha uongo. Biblia inakataza wanadamu kusema uongo.
Waefeso 4:25 ''Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.''
Kama umewahi kuzushiwa jambo baya ambalo wala hukulitenda naamini kabisa unajua madhara ya uongo.
Inawezekana wewe umezoea kusema uongo kila mara na kuona kuwa hiyo ni sawasawa tu, lakini ndugu naomba ujue kwamba uongo ni dhambi na hakuna mbingu ya waongo.
Nakuonya leo uachanae na uongo wako ili uanze kusema kweli maana ukweli ndicho kitu atakacho MUNGU.
Uongo hauna faida hata moja ila una hasara nyingi sana.
Kama wewe una mchumba na umezoea kumwambia uongo, siku akigundua kwamba usemacho ni uongo kwanza atakudharau na pili unaweza kuachwa maana wewe ni muongo.
Kuna watu huhubiri uongo kwa sababu wanaukataa wokovu wa KRISTO. Watu kama hao kwa mtu anayejielewa na anayemwelewa vizuri Mwokozi YESU hawawezi kuwasikiliza maana hawana kweli ndani yao.
Jiulize mfano mtumishi kanisani amefumaniwa harafu baada ya wiki 3 akaja akahuburi mbele yako, nauhakika atadhani unamdharau kumbe humwamini kwa sababu yeye ni muongo, hiyo ni hasara mojawapo ya uongo.
MUNGU anasema;
''Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.-Kutoka 23:1''
MUNGU anakataza uongo na pia anakataza watu wawe kuwa mashahidi wa jambo la uongo, ni dhambi.
Kunena uongo ni dhambi na Kunenewa Uongo Ni Kitu Kibaya Sana.
Uongo Ni Sumu Kali Inayoweza Kuangamiza.
Kuna watu wako jela leo sio kwa sababu walikosea bali ni kwa sababu ya kuzushiwa uongo.
Kuna watu leo hawana baba zao kwa sababu ya uongo wa mama zao enzi hizo. unakuta mama yule hakuna mwamini, alikuwa na wanaume zaidi ya moja na wakajua. Baada ya kuzaa kila mwanaume katika hao alikataa kwamba yule sio mtoto wake, hayo ni mojawapo ya madhara ya uongo katika jamii.
Kuna Watu Ndoa Zao Zina Vita Kila Siku Kwa Sababu Tu Ya Uongo Wa Jirani Au Ndugu Wa Karibu.
Kuna Wanawake Wameshindwa Kuolewa Kwa Sababu Tu Ya Uongo Waliozushiwa Na Watu Wa Karibu Yao. Uongo Huo Umekuwa Vazi Chakavu Walilovalishwa, Akija Tu Mtu Anayetaka Kumuoa Anaambiwa Huyo Binti Hajatulia, Anamwacha Na Kwenda Kuoa Mwingine.
Binti Hata Hajui Tatizo Ni Nini Hata Haolewi, Kumbe Amepakwa Matope Mengi Yaitwayo Uongo Ndio Yanayomzuia.
Biblia inaonya ikisema;
''Wala usimshuhudie jirani yako uongo.-Kumbukumbu 5:20''

Kuna Watu Hawaishi Kwa Amani Kazini Kwao Kwa Sababu Ya Uongo Wanaozushiwa.
Kuna Watu Hawana Raha katika Nyumba Wanazokaa Kwa Sababu Ya Kuzushiwa Uongo.
Uongo haujaanza leo ila ulikuwepo tangu zamani ambapo shetani aliwatumia walio wake kueneza uongo.
Kuna uongo ulienezwa zamani lakini watu wa siku hizi wanauishi uongo huo kutoka kwa shetani.
Mizimu ni kazi mojawapo ya kazi za shetani ili kudanganya ulimwengu. Leo kuna watu hutumia pesa zao mamilioni kwa ajili ya kutoa sadaka kwa mizimu ambayo hata haina msaada kwao hata mmoja, ila kwa kufuata ushauri wa mganga muongo, ndio maana watu wanapata ulaji kupitia utoaji huo kwa mizimu ambayo haina msaada hata mmoja kwa mwanadamu.
Uongo ni jambo baya sana.
Kuna watu leo kwenye maduka yao huweka udi na uvumba ili wapate wateja kumbe ni uongo wa shetani ili kufanya makazi kwao kupitoa majini.
Kuna watu akitoka nyumbani asubuhi anataka kila akikutana na mtu yeyote lazima yeye apite kushoto mwa yule aliyekutana naye, maana kama akipita kulia inajiona ana mkosi kumbe ni shetani katika ubora wake anadanganya wanadamu wasiojitambua na wasiotambua nguvu ya Muumba wao.
shetani ndiye baba wa uongo na anaposema uongo husema katika yaliyo yake maana kwake ni uongo tu daima.
Wanadamu wanaosema uongo Biblia inawaita watoto wa shetani ambaye ndiye mwasisi wa uongo.
Yohana 8:48 ''Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.''

Ndugu, je wewe unasema uongo au ukweli daima?
Kama unasema uongo baba yako ni shetani hivyo badilika leo kwa kuanza kusema ukweli tu ili ufanyike mteule wa MUNGU asiye na mawaa.
Kuna watu zamani ni kweli walikuwa wazinzi au wezi au wachawi sana ila waliookoka na kutubu na sasa wanaishi maisha matakatifu. lakini ni muhimu kuomba maombi ya kufuta uongo katika maisha yao maana kwa sasa wao hawauishi tena uongo bali wanaiishi kweli ya MUNGU.
Ndugu Zangu Japokuwa Watu Wanaweza Kukunenea Uongo Lakini Damu Ya YESU KRISTO Inaweza Kufuta Uongo Wote Ulionenewa Na Mtu Yeyote.
Walikupaka Matope Ya Uongo Lakini Kwa Maombi Yako BWANA Atakutakasa Na Kukuvika Vazi La Haki Kiasi Kwamba Mtu Akikusemea Uongo Kwa Watu Watamuona Yeye Ndiye Muongo. Jina YESU Kwa Maombi Litafuta Uongo Wote.
Kuna watu waliwahi kuzushiwa mambo mengi tu mabaya lakini kwenye ukweli siku zote uongo hujitenga.
Kuna hadi watumishi walizushiwa mambo mengi tu mabaya lakini kwa sababu uongo ni uongo tu na ukweli ni ukweli tu, uongo ulijitenga na ukweli ukabaki katika maisha yao.
Natamani kila anayekuzushia uongo basi uongo huo umrudie Yeye.
Nakuombea kila anayekuzushia uongo kazini kwako au katika harakati za usaili wa kupata kazi , uongo wake umvae mwenyewe na wewe ushinde kwa jina la YESU KRISTO.
1 Kor 10:14-15 ''Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.''

Kuna uongo mwingi sana uliofanywa zamani lakini wanadamu wa leo wanautendea kazi kana kwamba ni agizo la MUNGU kumbe uongo wa shetani.
Kuna watu wanaabudu sanamu wakidhani wanampendeza MUNGU kumbe ni machukizo.
Kuna watu wanasujudia mawe na miti wakidhani wanampendeza MUNGU kumbe ni machukizo makuu kwa MUNGU.
Kuna watu hutenga siku kadhaa katika kila mwaka ili kwenda kwa watu ambao wao huwaita ''watalaamu'' kutengeneza mambo yao kumbe huko ni kujikabidhi kwa shetani.
Uongo haufai na ni muhimu kila mwanadamu kujihadhari sana na uongo maana uongo ni dhambi na ni machukizo makuu.
Ibada ya sanamu ni ibada ya shetani na sio MUNGU.
Ibada ya sanamu ni ibada yeyote isiyo sahihi Kwa MUNGU aliye hai.
Biblia inasema;
''Kwa maana waliibadili kweli ya MUNGU kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.-Warumi 1:25''
Ibada ya sanamu ni kuabudu sanamu, kuabudu wanadamu, kuabudu shetani au kuabudu chochote kisicho MUNGU.
Wanadamu wengi tu wamenaswa katika kuabudu sanamu wakidhani ni mpango wa MUNGU kwao kumbe ni mpango wa shetani kwao.

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.